19 Mimi ni mmojawapo wa wale wanaopenda amani na uaminifu katika Israeli. Sasa wewe unakusudia kuuharibu mji ambao ni kama mama katika Israeli. Kwa nini sasa unataka kuuangamiza mji ulio mali yake Mwenyezi-Mungu?”
20 Yoabu akamjibu, “Kamwe maishani mwangu! Sina nia kuangamiza wala kuharibu.
21 Ulivyosema si kweli! Lakini mtu mmoja kutoka sehemu ya milima ya Efraimu aitwaye Sheba mwana wa Bikri anataka kumwasi mfalme Daudi. Mtoeni huyo kwangu nami nitaondoka mjini kwenu.” Yule mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake kitarushwa kwako kupitia ukutani.”
22 Kisha, huyo mwanamke akaenda kwa watu wote mjini kwa busara yake. Wakamkata kichwa Sheba mwana wa Bikri, wakakitupa nje kwa Yoabu. Kwa hiyo, Yoabu akapiga tarumbeta, na kuwatawanya watu wake kutoka mji huo wa Abeli; kila mtu akaenda nyumbani kwake. Kisha Yoabu akarudi kwa mfalme Daudi, mjini Yerusalemu.
23 Sasa Yoabu alikuwa mkuu wa jeshi lote la Israeli. Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa mkuu wa Wakerethi na Wapelethi.
24 Adoramu alikuwa msimamizi wa kazi za kulazimishwa; Yehoshafati alikuwa mwandishi wa kumbukumbu.
25 Shausha alikuwa katibu; Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani.