5 Huko Hebroni, alitawala watu wa Yuda kwa muda wa miaka saba na miezi sita, na huko Yerusalemu alitawala watu wa Israeli pamoja na Yuda kwa muda wa miaka thelathini na mitatu.
6 Baadaye mfalme na watu wake walikwenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo. Lakini wao wakamwambia, “Hutaingia mjini humu, kwani vipofu na vilema watakufukuzia mbali.” Walimwambia hivyo kwani walifikiri kuwa Daudi asingeweza kuingia mjini humo.
7 Hata hivyo, mfalme Daudi aliiteka ngome ya Siyoni, yaani mji wa Daudi.
8 Siku hiyo, Daudi alisema, “Mtu yeyote atakayewapiga Wayebusi na apitie kwenye mfereji wa maji ili kuwashambulia vilema na vipofu ambao roho yangu inawachukia.” Ndio maana watu husema, “Vipofu na vilema hawataingia nyumbani.”
9 Daudi alikaa kwenye ngome hiyo, nao mji akauita, “Mji wa Daudi.” Daudi aliujenga mji kuuzunguka, akianzia Milo kuelekea ndani.
10 Naye Daudi akazidi kuwa maarufu zaidi kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye.
11 Kisha, mfalme Hiramu wa Tiro alituma wajumbe kwa Daudi; alimpelekea pia mierezi, maseremala na waashi ambao walimjengea Daudi ikulu.