16 Ukoo wako na ufalme wako vitadumu imara daima. Kiti chako cha enzi kitakuwa imara milele.’”
17 Nathani alimweleza Daudi kila kitu ambacho alioneshwa katika maono hayo na Mungu.
18 Kisha mfalme Daudi akaingia ndani na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu; halafu akaomba, “Mimi ni nani ee Bwana Mungu, na jamaa yangu ni nini hata ukaniinua mpaka hapa nilipo leo!
19 Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Bwana Mungu; zaidi ya hayo umeiahidi jamaa yangu mambo makubwa katika miaka mingi ijayo; na kwamba umenijalia kuona hayo, Ee Bwana Mungu.
20 Nikuambie nini zaidi, mimi Daudi, mtumishi wako? Kwani wewe unanijua mimi mtumishi wako, ee Bwana Mungu!
21 Kutokana na ahadi yako na kulingana na moyo wako, umetenda makuu hayo yote ili unijulishe mimi mtumishi wako.
22 Kutokana na yale tuliyosikia, wewe Mwenyezi-Mungu ni mkuu; hakuna aliye kama wewe, na hakuna Mungu mwingine ila wewe.