Danieli 4:17-23 BHN

17 Hii ni hukumu iliyotangazwa na walinzi; ni uamuzi wa walio watakatifu, ili wanaadamu wote kila mahali wapate kutambua kuwa Mungu Mkuu anayo mamlaka juu ya falme zote za wanaadamu; yeye humpa ufalme mtu yeyote ampendaye, humfanya mfalme hata mtu duni wa mwisho.’

18 “Hii ndiyo ndoto niliyoota mimi Nebukadneza. Sasa, wewe Belteshaza, nieleze maana yake; kwani wenye hekima wote katika ufalme wangu hawawezi kuniambia maana yake; lakini wewe utaweza kwa kuwa roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako.”

19 Hapo, Danieli, aliyeitwa pia Belteshaza, akashangaa kwa muda, na fikira zake zikamfadhaisha. Mfalme akamwambia, “Belteshaza, ndoto hii, wala maana yake visikufadhaishe!” Belteshaza akamjibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii na maana yake ingewahusu adui zako!

20 Mti uliouona ukiwa mkubwa na wenye nguvu, ambao matawi yake marefu yalifika mbinguni, nao ukionekana kutoka kila mahali duniani,

21 majani yake yakiwa mazuri, na matunda yake mengi ya kulisha viumbe vyote, wanyama wa porini wakipata kivuli chini yake, na ndege wa angani wakikaa katika matawi yake,

22 basi, ni wewe ee mfalme ambaye umekuwa mkubwa na mwenye nguvu. Ukuu wako umefika mpaka mbinguni, na ufalme wako umeenea mpaka miisho ya dunia.

23 Kisha ukaona tena, ee mfalme, Mlinzi mtakatifu akishuka kutoka mbinguni, akaamuru: ‘Ukateni mti huu, mkauangamize. Lakini acheni kisiki chake na mizizi yake ardhini kwenye majani mabichi ya kondeni, kikiwa kimefungwa hapo kwa mnyororo wa chuma na shaba. Mwacheni mtu huyo aloweshwe kwa umande wa mbinguni; mwacheni aishi pamoja na wanyama wa porini kwa miaka saba.’