1 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Tazama, siku yaja, nayo inawaka kama tanuri. Wenye kiburi na waovu wote watatupwa humo na kuteketea kama mabua makavu; watateketea kabisa pasibaki hata alama.
2 Lakini kwa ajili yenu nyinyi mnaonicha, uwezo wangu wa kuokoa utawachomozea kama jua lililo na nguvu za kuponya kwenye mionzi yake. Mtatoka mkirukaruka kama ndama watokapo zizini mwao.
3 Siku hiyo mtawakanyagakanyaga waovu, nao watakuwa kama majivu chini ya nyayo zenu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
4 “Kumbukeni sheria, kanuni na maagizo yangu niliyomwamuru Mose mtumishi wangu kule mlimani Horebu, ili awaamuru watu wote wa Israeli.