13 Ruthu akamjibu, “Bwana, wewe umenifanyia wema mkubwa sana. Ingawa mimi si kama mmoja wa watumishi wako, nimeridhika kwa kuwa umenifariji sana na kuongea nami kwa ukarimu.”
14 Wakati wa chakula, Boazi alimkaribisha Ruthu akamwambia, “Karibu hapa, njoo ule mkate pia na uuchovye ndani ya divai.” Kwa hiyo Ruthu akaketi pamoja na wavunaji, na Boazi akampa nafaka iliyokaangwa, akala akashiba hata akabakiza.
15 Na ikawa Ruthu alipoendelea kuokota mavuno, Boazi aliwaambia wafanyakazi wake, “Mwacheni akusanye hata mahali miganda ilipo wala msimkemee.
16 Zaidi ya hapo, vuteni masuke kutoka katika matita na mumwachie aokote bila kumkaripia.”
17 Basi Ruthu aliendelea kuokota masuke mpaka jioni; na baada ya kupura hiyo shayiri alipata debe moja na zaidi.
18 Kisha akachukua mavuno hayo hadi mjini na kumwonesha mama mkwe wake kiasi alichookota. Pia alikitoa kile chakula alichobakiza baada ya kushiba, akampa.
19 Basi mkwewe akamwuliza, “Uliokota wapi haya yote? Je, ulikuwa katika shamba la nani? Heri huyo aliyekufadhili.” Hapo Ruthu akamwambia Naomi kwamba alikuwa amefanya kazi katika shamba la mtu aliyeitwa Boazi.