1 Wafuatao ndio wafalme ambao Waisraeli waliwashinda na kuchukua nchi yao yote iliyokuwa mashariki ya mto Yordani kutoka bonde la mto Arnoni mpaka mlima Hermoni na nchi yote ya Araba upande wa mashariki:
2 Mfalme Sihoni wa Waamori aliyeishi huko Heshboni na kutawala kutoka makao yake makuu huko Aroeri, mji uliokuwa kandokando ya bonde la Arnoni. Alitawala pia kuanzia katikati ya bonde hadi mto Yaboki ambao ulikuwa mpaka wa nchi ya Waamoni, yaani nusu ya nchi ya Gileadi.
3 Vilevile, alitawala nchi yote ya Araba, kutoka bahari ya Kinerethi, upande wa mashariki, mpaka Beth-yeshimothi kwenye Bahari ya Chumvi na kuendelea mpaka chini ya mlima Pisga.
4 Mwingine ni mfalme Ogu mmoja wa Warefai waliosalia, ambaye alitawala Bashani na alikaa Ashtarothi au Edrei.
5 Utawala wake ulienea huko kwenye mlima Hermoni, huko Saleka, Bashani yote mpaka mipaka ya Wageshuri na Wamaaka, nusu ya Gileadi hadi mpakani mwa nchi ya mfalme Sihoni wa Heshboni.
6 Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, pamoja na Waisraeli aliwashinda wafalme hao, akayapatia nchi hizo makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase ziwe mali yao kabisa.
7 Kisha Yoshua pamoja na Waisraeli waliwashinda wafalme wote wa eneo lote lililoko magharibi ya mto Yordani, kuanzia Baal-gadi katika bonde la Lebanoni mpaka mlima uliokuwa mtupu wa Halaki kusini karibu na Seiri. Yoshua akayagawia makabila ya Israeli nchi hizo ziwe mali yao kabisa.
8 Nchi hizo zilikuwa pamoja na maeneo ya milima, nchi tambarare, eneo la Araba, miteremko ya milima, maeneo ya nyika, na eneo la Negebu; nchi zilizokuwa za Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.
9 Wafalme waliowashinda walikuwa, mmojammoja: Mfalme wa Yeriko, mfalme wa Ai mji ulioko karibu na Betheli,
10 mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni,
11 mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi,
12 mfalme wa Egloni, mfalme wa Gezeri,
13 mfalme wa Debiri, mfalme wa Gederi,
14 mfalme wa Horma, mfalme wa Aradi,
15 mfalme wa Libna, mfalme wa Adulamu,
16 mfalme wa Makeda, mfalme wa Betheli,
17 mfalme wa Tapua, mfalme wa Heferi,
18 mfalme wa Afeka, mfalme wa Lasharoni,
19 mfalme wa Madoni, mfalme wa Hazori,
20 mfalme wa Shimron-meroni, mfalme wa Akshafi,
21 mfalme wa Taanaki, mfalme wa Megido,
22 mfalme wa Kedeshi, mfalme wa Yokneamu mji ulioko kwenye mlima Karmeli,
23 mfalme wa Dori katika mkoa wa Nafath-dori, mfalme wa Goiimu huko Gilgali na
24 mfalme wa Tirza. Jumla ya wafalme hao ni thelathini na mmoja.