1 Baada ya kuishinda ile nchi, jumuiya yote ya Waisraeli ilikusanyika huko Shilo na kulisimika hema la mkutano.
2 Yalikuwa yamebaki kati yao makabila saba ambayo hayakuwa yamegawiwa sehemu yao ya nchi.
3 Kwa hiyo, Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtakawia mpaka lini kwenda kuimiliki nchi ile ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, amewapeni?
4 Chagueni watu watatu kutoka kila kabila niwatume nchini kote wachunguze na kuchora ramani kulingana na makabila yao, kisha waniletee taarifa.
5 Nao wataigawanya nchi hiyo sehemu saba. Kabila la Yuda litabaki na sehemu yake ya kusini na kabila la Yosefu kaskazini.