3 Kwa hiyo, Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtakawia mpaka lini kwenda kuimiliki nchi ile ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, amewapeni?
4 Chagueni watu watatu kutoka kila kabila niwatume nchini kote wachunguze na kuchora ramani kulingana na makabila yao, kisha waniletee taarifa.
5 Nao wataigawanya nchi hiyo sehemu saba. Kabila la Yuda litabaki na sehemu yake ya kusini na kabila la Yosefu kaskazini.
6 Tayarisheni maelezo kamili juu ya sehemu zote saba na kuniletea. Hapo, nitapiga kura mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kuhusu sehemu ya kila kabila lenu.
7 Lakini Walawi hawatapata sehemu yoyote kati yenu, maana sehemu yao ni kuwa makuhani wa kumhudumia Mwenyezi-Mungu. Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase walikwisha pata sehemu yao upande wa mashariki wa mto Yordani. Walipewa sehemu hii na Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu.”
8 Basi, watu hao wakaanza safari ya kwenda kuichunguza nchi. Kabla hawajaenda, Yoshua akawapa maagizo: “Nendeni nchini kote mkaandike maelezo kamili juu ya hiyo nchi, kisha mrudi mnieleze, nami nitapiga kura mbele ya Mwenyezi-Mungu hapa hapa Shilo kuhusu sehemu mtakayopewa.”
9 Wanaume hao wakazunguka nchini kote, wakachora maelezo kamili juu ya sehemu zake saba pamoja na miji yake, kisha wakarudi kwa Yoshua kule kambini Shilo.