5 Yoshua akawaambia watu, “Jitakaseni kwa kuwa kesho Mwenyezi-Mungu atatenda maajabu kati yenu.”
6 Kisha akawaambia makuhani, “Chukueni sanduku la agano, mtangulie nalo mbele ya watu.” Nao wakalichukua na kutangulia mbele ya watu.
7 Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua: “Leo hii, nitaanza kukutukuza mbele ya watu wote wa Israeli ili wajue kwamba, kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo pia nitakavyokuwa pamoja nawe.
8 Utawaamuru hao makuhani wanaobeba sanduku la agano wasimame karibu na ukingo wa mto Yordani wakati watakapofika huko.”
9 Kisha Yoshua akawaambia Waisraeli: “Njoni karibu mpate kusikia maneno ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”
10 Yoshua akaendelea kusema, “Sasa mtajulishwa kabisa kwamba Mungu aliye hai yu miongoni mwenu na kwamba atawafukuza mbele yenu Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi, bila kushindwa.
11 Tazameni, sanduku la agano la Bwana wa dunia yote, liko karibu kupita mbele yenu kuelekea mtoni Yordani.