3 uwaagize hivi, ‘Chukueni mawe kumi na mawili kutoka hapa katikati ya mto Yordani, kutoka hapa ilipo miguu ya makuhani, muyachukue mawe hayo, mkayaweke mahali pale ambapo mtalala leo hii.’”
4 Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili ambao alikuwa amewateua miongoni mwa Waisraeli, kila kabila mtu mmoja,
5 akawaambia, “Litangulieni sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mpaka katikati ya mto Yordani. Kila mmoja wenu achukue jiwe begani mwake, jiwe moja kwa ajili ya kila kabila la Israeli.
6 Jambo hilo litakuwa ishara kati yenu; na watoto wenu watakapowauliza siku zijazo ‘Je, mawe haya yana maana gani kwenu?’
7 Nyinyi mtawaambia, ‘Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipopitishwa mtoni Yordani, maji ya mto huo yalizuiliwa yasitiririke!’ Kwa hiyo mawe haya yatakuwa ukumbusho kwa Waisraeli milele.”
8 Wale wanaume wakafanya kama walivyoamriwa na Yoshua, wakachukua mawe kumi na mawili kutoka katikati ya mto Yordani, jiwe moja kwa ajili ya kila kabila la Israeli, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Yoshua, wakaenda nayo hadi mahali pale walipolala, wakayaweka huko.
9 Yoshua akasimika pia mawe kumi na mawili katikati ya mto Yordani, mahali pale ambapo nyayo za makuhani waliobeba lile sanduku la agano zilisimama. Mawe hayo yako huko mpaka hivi leo.