11 Wanajeshi wote waliofuatana naye walikaribia mji na kupiga kambi kaskazini yake, ngambo ya bonde mkabala wa mji wa Ai.
12 Ndipo akachukua watu wengine 5,000 na kuwaweka wavizie kati ya mji wa Betheli na Ai, magharibi ya mji wa Ai.
13 Kikosi kikubwa kiliwekwa kaskazini mwa mji na wale waliobaki waliwekwa magharibi ya mji. Lakini usiku huo, Yoshua akalala bondeni.
14 Mfalme wa mji wa Ai alipoona hivyo, aliharakisha na kwenda kwenye mteremko wa kuelekea Araba ili akabiliane na Waisraeli vitani. Lakini hakujua kwamba mji wake ulikuwa umeviziwa kutoka nyuma.
15 Kisha Yoshua pamoja na watu wake wakajifanya kana kwamba wanashindwa, wakaanza kukimbia kuelekea jangwani.
16 Watu wote waliokuwa mjini waliitwa wawafuatie Waisraeli; na walipokuwa wanamfuatia Yoshua, walitoka na kwenda mbali na mji wao.
17 Hakuna mtu yeyote aliyebaki mjini Ai, waliuacha mji huo wazi wakaenda kuwafuatia Waisraeli.