1 Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana.
2 Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu.
3 Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati;
4 kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;
5 si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu.
6 Mtu asimpunje ndugu yake wala kumkosa katika jambo hili; kwa sababu Bwana ndiye alipizaye kisasi cha haya yote; kama tulivyowaambia kwanza, tukashuhudia sana.