1 Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu;
2 wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote.
3 Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli.
4 Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu.
5 Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.
6 Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai.
7 Mambo hayo pia uyaagize, ili wasiwe na lawama.