1 Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu;
2 tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani.
3 Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu.
4 Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tulivyowaagiza, tena kwamba mtayafanya.
5 Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na saburi ya Kristo.
6 Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu.
7 Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu;
8 wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote.
9 Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate.
10 Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.
11 Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine.
12 Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe.
13 Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema.
14 Na ikiwa mtu awaye yote halishiki neno letu la waraka huu, jihadharini na mtu huyo, wala msizungumze naye, apate kutahayari;
15 lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.
16 Sasa, Bwana wa amani mwenyewe na awape amani daima kwa njia zote. Bwana awe pamoja nanyi nyote.
17 Salamu zangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndiyo alama katika kila waraka, ndio mwandiko wangu.
18 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote.