2 kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.
3 Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana.
4 Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha;
5 nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo.
6 Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.
7 Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.
8 Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu;