1 Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,
2 mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.
3 Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;
4 amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.
5 Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote,Ndiwe mwanangu,Mimi leo nimekuzaa?Na tenaMimi nitakuwa kwake baba,Na yeye atakuwa kwangu mwana?
6 Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema,Na wamsujudu malaika wote wa Mungu.
7 Na kwa habari za malaika asema,Afanyaye malaika wake kuwa pepo,Na watumishi wake kuwa miali ya moto.
8 Lakini kwa habari za Mwana asema,Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele;Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili.
9 Umependa haki, umechukia maasi;Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta,Mafuta ya shangwe kupita wenzio.
10 Na tena,Wewe, Bwana, hapo mwanzo uliitia misingi ya nchi,Na mbingu ni kazi za mikono yako;
11 Hizo zitaharibika, bali wewe unadumu;Nazo zote zitachakaa kama nguo,
12 Na kama mavazi utazizinga, nazo zitabadilika;Lakini wewe u yeye yule,Na miaka yako haitakoma.
13 Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo wote,Uketi mkono wangu wa kuumeHata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako?
14 Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?