15 Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli.
16 Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu.
17 Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu.
18 Mara vikaanguka machoni pake vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa;
19 akala chakula, na kupata nguvu.Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski.
20 Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu.
21 Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, Siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa alikuwa amekuja kwa kusudi hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani?