18 na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze.
19 Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu.
20 Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini, akagaa-gaa, akitokwa na povu.
21 Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, Tangu utoto.
22 Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia.
23 Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.
24 Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu.