1 Hata walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake,
2 akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwana-punda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni.
3 Na mtu akiwaambia, Mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana anamhitaji na mara atamrudisha tena hapa.
4 Wakaenda zao, wakamwona mwana-punda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua.
5 Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwana-punda?
6 Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu.
7 Wakamletea Yesu yule mwana-punda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake.
8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani.
9 Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana;
10 umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni.
11 Naye akaingia Yerusalemu hata ndani ya hekalu; na alipokwisha kutazama yote pande zote, kwa kuwa ni wakati wa jioni, akatoka, akaenda Bethania pamoja na wale Thenashara.
12 Hata asubuhi yake walipotoka Bethania aliona njaa.
13 Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini.
14 Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia.
15 Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa;
16 wala hakuacha mtu achukue chombo kati ya hekalu.
17 Akafundisha, akasema, Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.
18 Wakuu wa makuhani na waandishi wakapata habari wakatafuta jinsi ya kumwangamiza; maana walimwogopa, kwa sababu mkutano wote walishangaa kwa mafundisho yake.
19 Na kulipokuwa jioni alitoka mjini.
20 Na asubuhi walipokuwa wakipita, waliuona ule mtini umenyauka toka shinani.
21 Petro akakumbuka habari yake, akamwambia, Rabi, tazama, mtini ulioulaani umenyauka.
22 Yesu akajibu, akamwambia, Mwaminini Mungu.
23 Amin, nawaambia, Ye yote atakayeuambia mlima huu, Ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake.
24 Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.
25 Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. [
26 Lakini kama ninyi hamsamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]
27 Wakafika Yerusalemu tena; hata alipokuwa akitembea hekaluni, walimwendea wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee,
28 wakamwambia, Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya?
29 Yesu akawaambia, Nitawauliza neno moja, nanyi mnijibu, kisha nitawaambia ni kwa mamlaka gani nayatenda haya.
30 Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Nijibuni.
31 Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini?
32 Ila tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, – waliogopa watu; maana watu wote walimwona Yohana kuwa nabii halisi.
33 Wakamjibu Yesu, wakasema, Hatujui. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani nayatenda haya.