4 Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu.
5 Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.
6 Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi.
7 Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.
8 Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake.
9 Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu.
10 Wakalishika neno lile, wakiulizana wao kwa wao, Huko kufufuka katika wafu maana yake nini?