3 Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu.
4 Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi;
5 tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,
6 na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.
7 Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina.
8 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.
9 Mimi Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu.