1 Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwana-Kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao.
2 Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni, kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu. Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao;
3 na kuimba wimbo mpya mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya wale wenye uhai wanne, na wale wazee; wala hapana mtu aliyeweza kujifunza wimbo ule, ila wale mia na arobaini na nne elfu, walionunuliwa katika nchi.
4 Hawa ndio wasiotiwa unajisi pamoja na wanawake, kwa maana ni bikira. Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.
5 Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa.
6 Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa,
7 akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.