1 Malaika wa tano akapiga baragumu, nikaona nyota iliyotoka mbinguni, imeanguka juu ya nchi; naye akapewa ufunguo wa shimo la kuzimu.
2 Akalifungua shimo la kuzimu; moshi ukapanda kutoka mle shimoni kama moshi wa tanuru kubwa; jua na anga vikatiwa giza kwa sababu ya ule moshi wa shimoni.
3 Nzige wakatoka katika ule moshi, wakaenda juu ya nchi, wakapewa nguvu kama nguvu waliyo nayo nge wa nchi.
4 Wakaambiwa wasiyadhuru majani ya nchi, wala kitu cho chote kilicho kibichi, wala mti wo wote, ila wale watu wasio na muhuri ya Mungu katika vipaji vya nyuso zao.
5 Wakapewa amri kwamba wasiwaue, bali wateswe miezi mitano. Na maumivu yao yalikuwa kama kuumwa na nge, aumapo mwanadamu.
6 Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia.