6 Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.
7 Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa Bwana.
8 Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote.
9 Lakini ndugu asiye na cheo na afurahi kwa kuwa ametukuzwa;
10 bali tajiri kwa kuwa ameshushwa; kwa maana kama ua la majani atatoweka.
11 Maana jua huchomoza kwa hari, huyakausha majani; ua lake huanguka, uzuri wa umbo lake hupotea; vivyo hivyo naye tajiri atanyauka katika njia zake.
12 Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.