1 Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu.
2 Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu;
3 nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu,
4 je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu?
5 Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao?
6 Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu?
7 Hawalitukani jina lile zuri mliloitwa?
8 Lakini mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa, Mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vema.
9 Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji.
10 Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote.
11 Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria.
12 Semeni ninyi, na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ya uhuru.
13 Maana hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu.
14 Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa?
15 Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki,
16 na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini?
17 Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake.
18 Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu.
19 Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka.
20 Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?
21 Je! Baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu?
22 Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale.
23 Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu.
24 Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake.
25 Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine?
26 Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa.