4 Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia.Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi.
5 Lakini sasa mimi naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwendapi?
6 Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu.
7 Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.
8 Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.
9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi;
10 kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena;