21 Naye Hadadi aliposikia huko Misri ya kuwa Daudi amelala na babaze, na Yoabu, jemadari wa jeshi, amekufa, Hadadi akamwambia Farao, Unipe ruhusa, niende mpaka nchi yangu.
22 Farao akamwambia, Umekosa nini kwangu, hata, tazama, unatafuta kuirudia nchi yako? Akajibu, Hakuna, lakini unipe ruhusa tu.
23 Tena, Mungu akamwondokeshea adui mwingine, Rezoni mwana wa Eliada, aliyemkimbia bwana wake Hadadezeri mfalme wa Soba,
24 naye akakusanya watu, akawa mkuu wa jeshi, hapo Daudi alipowaua hao watu wa Soba; wakaenda Dameski, wakakaa humo, na kumiliki huko Dameski.
25 Naye akawa adui wa Israeli siku zote za Sulemani, zaidi ya madhara yake Hadadi; naye akawachukia Israeli, akamiliki juu ya Shamu.
26 Na Yeroboamu wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumwa wake Sulemani; ambaye jina lake mamaye aliitwa Serua, mwanamke aliyefiwa na mumewe; yeye naye akainua mkono wake juu ya mfalme.
27 Na hii ndiyo sababu ya yeye kumwinulia mfalme mkono. Sulemani aliijenga Milo, akapafunga palipobomoka pa mji wa baba yake Daudi.