22 Lakini likaja neno la Mungu kwa Shemaya mtu wa Mungu, kusema,
23 Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, na jamaa yote ya Yuda na Benyamini, na watu waliosalia, ukisema,
24 BWANA asema hivi, Msiende, wala msipigane na ndugu zenu wana wa Israeli; rudini kila mtu nyumbani kwake; kwa kuwa jambo hili limetoka kwangu. Basi, wakalisikiliza neno la BWANA, wakarudi, wakaenda zao, sawasawa na neno la BWANA.
25 Ndipo Yeroboamu akajenga Shekemu katika milima ya Efraimu, akakaa huko. Akatoka huko akajenga Penueli.
26 Yeroboamu akasema moyoni mwake, Basi ufalme utairudia nyumba ya Daudi.
27 Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya BWANA huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu hawa itamrudia bwana wao, yaani Rehoboamu, mfalme wa Yuda; nao wataniua mimi, na kumrudia Rehoboamu, mfalme wa Yuda.
28 Kwa hiyo mfalme akafanya shauri, akafanyiza ng’ombe wawili wa dhahabu, akawaambia watu, Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri.