25 Ndipo Yeroboamu akajenga Shekemu katika milima ya Efraimu, akakaa huko. Akatoka huko akajenga Penueli.
26 Yeroboamu akasema moyoni mwake, Basi ufalme utairudia nyumba ya Daudi.
27 Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya BWANA huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu hawa itamrudia bwana wao, yaani Rehoboamu, mfalme wa Yuda; nao wataniua mimi, na kumrudia Rehoboamu, mfalme wa Yuda.
28 Kwa hiyo mfalme akafanya shauri, akafanyiza ng’ombe wawili wa dhahabu, akawaambia watu, Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri.
29 Akamweka mmoja katika Betheli, na wa pili akamweka katika Dani.
30 Jambo hili likawa dhambi, maana watu walikwenda kuabudu mbele ya kila mmoja, hata huko Dani.
31 Tena akafanya nyumba za mahali pa juu, akafanya na watu wo wote, watu wasio wa wana wa Lawi, kuwa makuhani.