13 Akawaambia wanawe, Nitandikieni punda. Wakamtandikia punda, naye akampanda.
14 Akamfuata mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mwaloni, akamwambia, Je! Wewe ndiwe yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda? Akamwambia, Mimi ndiye.
15 Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula.
16 Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa;
17 kwani nimeambiwa kwa neno la BWANA, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
18 Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la BWANA, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo.
19 Basi mtu yule akarudi pamoja naye, akala chakula, akanywa maji nyumbani mwake.