26 Na yule nabii aliyemrudisha njiani alipopata habari, akasema; Ndiye yule mtu wa Mungu, aliyeiasi kauli ya BWANA; kwa hiyo BWANA amempambanisha na simba, simba akamrarua, akamwua, sawasawa na neno la BWANA alilomwambia.
27 Akawaambia wanawe, akasema, Nitandikieni punda. Wakamtandikia.
28 Akaenda, akamwona yule maiti ametupwa njiani, na punda na simba wamesimama karibu na maiti; yule simba alikuwa hakumla maiti, wala hakumrarua punda.
29 Nabii yule akamtwaa maiti wa yule mtu wa Mungu, akamweka juu ya punda wake, akamrudisha; yule nabii mzee akaenda mjini mwake, kukaa matanga, na kumzika.
30 Akamweka maiti katika kaburi lake mwenyewe; wakamlilia, wakisema, Aa! Ndugu yangu!
31 Hata ikawa, alipokwisha kumzika, akawaambia wanawe, akasema, Nikifa mimi, nizikeni katika kaburi hili alimozikwa yule mtu wa Mungu; iwekeni mifupa yangu kando ya mifupa yake.
32 Kwa maana neno hilo alilolia juu ya madhabahu katika Betheli, kwa neno la BWANA, na juu ya nyumba zote za mahali pa juu zilizo katika miji ya Samaria, hakika litatimizwa.