15 Kwa kuwa BWANA atawapiga Israeli kama manyasi yatikiswavyo majini; naye atawang’oa Israeli katika nchi hii njema, aliyowapa baba zao, naye atawatawanya ng’ambo ya Mto; kwa sababu wamejifanyia maashera yao, wakimkasirisha BWANA.
16 Naye atawatoa Israeli kwa ajili ya makosa ya Yeroboamu, aliyoyakosa, ambayo kwa hayo amewakosesha Israeli.
17 Basi mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda zake, akafika Tirza; naye alipofika kizingitini kwa nyumba, huyo kijana akafa.
18 Israeli wote wakamzika, wakamlilia; sawasawa na neno la BWANA, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Ahiya nabii.
19 Na mambo yake Yeroboamu yaliyosalia, ya kupigana na ya kutawala, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.
20 Na siku alizotawala Yeroboamu zilikuwa miaka ishirini na miwili; akalala na babaze, naye Nadabu mwanawe akatawala mahali pake.
21 Naye Rehoboamu mwana wa Sulemani akatawala katika Yuda. Rehoboamu akaanza kutawala alipokuwa mwenye miaka arobaini na mmoja, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua BWANA miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke jina lake huko. Na jina la mamaye aliitwa Naama, Mwamoni.