6 Ikawa, Ahiya alipoisikia sauti ya miguu yake, akiingia mlangoni, alisema, Karibu, mkewe Yeroboamu; mbona wajifanya kuwa mwingine maana nimetumwa kwako wewe, mwenye maneno mazito.
7 Nenda, umwambie Yeroboamu, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa nilikutukuza miongoni mwa watu, nikakufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli,
8 nikaurarulia mbali ufalme utoke nyumba yake Daudi, na kukupa wewe; walakini wewe hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, aliyezishika amri zangu, na kunifuata kwa moyo wake wote, asifanye lo lote ila yaliyo mema machoni pangu;
9 lakini umekosa kuliko wote waliokutangulia, umekwenda kujifanyia miungu mingine, na sanamu zilizoyeyuka, unikasirishe, na kunitupa nyuma yako;
10 tazama, kwa hiyo mimi nitaleta mabaya juu ya nyumba yake Yeroboamu, nami nitamkatia Yeroboamu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli, nami kuondoa nitawaondoa waliobaki wa nyumba yake Yeroboamu, kama mtu aondoavyo mavi, hata itakapokwisha pia.
11 Yeye afaye wa Yeroboamu mjini mbwa watamla; afaye mashambani ndege wa angani watamla; kwa kuwa BWANA amelinena hilo.
12 Basi ondoka, urudi nyumbani kwako; na miguu yako itakapoingia mjini huyo kijana atakufa.