25 Nadabu mwana wa Yeroboamu alianza kutawala juu ya Israeli, mwaka wa pili wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala juu ya Israeli miaka miwili.
26 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, akaiendea njia ya baba yake, na kosa lake alilowakosesha Israeli.
27 Basi Baasha wa Ahiya, wa mbari ya Isakari, akamfanyia fitina; Baasha akampiga huko Gibethoni ulio wa Wafilisti; kwani Nadabu na Israeli wote walikuwa wakiuhusuru Gibethoni.
28 Mwaka wa tatu wa Asa mfalme wa Yuda Baasha akamwua, akatawala mahali pake.
29 Ikawa mara alipotawala, akawapiga nyumba yote ya Yeroboamu. Hakumwachia Yeroboamu mwenye pumzi ye yote, hata alipomharibu sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa mtumishi wake Ahiya, Mshiloni;
30 kwa sababu ya makosa yake Yeroboamu aliyoyakosa, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; kwa sababu ya chukizo lake alilomchukiza BWANA, Mungu wa Israeli, hata kumghadhibisha.
31 Basi mambo yote ya Nadabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?