10 Zimri akaingia akampiga, akamwua, katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala mahali pake.
11 Ikawa, alipoanza kutawala, mara alipoketi juu ya kiti chake cha enzi, akawaua nyumba yote ya Baasha; hakumwachia mwanamume ye yote, wa jamaa zake, wala wa rafiki zake.
12 Hivyo Zimri akaiharibu nyumba yote ya Baasha, sawasawa na neno la BWANA, alilolinena juu ya Baasha kwa Yehu nabii,
13 kwa sababu ya makosa yake Baasha, na makosa yote ya Ela mwanawe, waliyoyakosa, na kuwakosesha Israeli, wakimghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili.
14 Na mambo yote ya Ela yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
15 Katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala muda wa siku saba huko Tirza. Basi, watu walikuwa wametua maragoni kupigana na Gibethoni, ulio wa Wafilisti.
16 Na hao watu waliokuwako maragoni wakasikia habari ya kwamba Zimri amefanya fitina, tena amempiga mfalme; kwa hiyo Israeli wote wakamfanya Omri, jemadari wa jeshi, awe mfalme juu ya Israeli siku ile maragoni.