2 Kwa kuwa mimi nilikuinua kutoka katika mavumbi, na kukufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli; nawe umeiendea njia ya Yeroboamu, na kuwakosesha watu wangu Israeli, hata wanighadhibishe kwa makosa yao;
3 angalia, kuondoa nitawaondoa Baasha na jamaa yake; tena nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati.
4 Mtu amfiaye Baasha mjini mbwa watamla; naye amfiaye mashambani ndege wa angani watamla.
5 Basi, mambo yote ya Baasha yaliyosalia, na aliyoyafanya, na nguvu zake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
6 Baasha akalala na babaze, akazikwa katika Tirza; naye Ela mwanawe akatawala mahali pake.
7 Tena neno la BWANA likaja kwa mkono wa nabii Yehu mwana wa Hanani juu ya Baasha, na juu ya nyumba yake, kwa sababu ya mabaya yote aliyoyatenda machoni pa BWANA, akimghadhibisha kwa kazi ya mikono yake, kwa kufanana na nyumba ya Yeroboamu, na kwa sababu aliiharibu.
8 Katika mwaka wa ishirini na sita wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha alianza kutawala juu ya Israeli huko Tirza, akatawala miaka miwili.