32 Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu.
33 Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni.
34 Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu.
35 Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji.
36 Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.
37 Unisikie, Ee BWANA, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, BWANA, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.
38 Ndipo moto wa BWANA ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.