1 Basi siku ya kufa kwake Daudi ikakaribia, akamwusia Sulemani mwanawe, akasema,
2 Mimi naenda njia ya ulimwengu wote; basi uwe hodari, ujionyeshe kuwa mwanamume;
3 uyashike mausia ya BWANA, Mungu wako, uende katika njia zake, uzishike sheria zake, na amri zake, na hukumu zake, na shuhuda zake, sawasawa na ilivyoandikwa katika torati ya Musa, upate kufanikiwa katika kila ufanyalo, na kila utazamako;
4 ili BWANA afanye imara neno lake alilonena kwa habari yangu, akisema, Ikiwa watoto wako wataiangalia njia yao, wakienda mbele zangu kwa kweli, kwa moyo wao wote, na kwa roho yao yote, (akasema), hutakosa mtu katika kiti cha enzi cha Israeli.
5 Na zaidi ya hayo, umejua alivyonitenda Yoabu, mwana wa Seruya, yaani, alivyowatenda majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri, mwana wa Neri, na Amasa, mwana wa Yetheri, ambao aliwaua, na kuimwaga damu ya vita wakati wa amani, akautia damu ya vita mshipi uliokuwa viunoni mwake, na viatu vilivyokuwa miguuni mwake.
6 Kwa hiyo ufanye kama ilivyo hekima yako, wala usimwachie mvi zake kushukia Ahera kwa amani.