13 Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akaja kwa Bath-sheba mamaye Sulemani. Naye akasema, Je! Umekuja kwa amani?
14 Naye akajibu, Kwa amani. Tena akasema, Nina shauri ninalotaka kukuambia. Naye akamwambia, Sema.
15 Basi akasema, Wajua ya kwamba ufalme ulikuwa wangu, na Israeli wote wakaniwekea nyuso zao ili nimiliki mimi; walakini sasa ufalme umegeuka kuwa wake ndugu yangu; kwa maana ulikuwa wake kutoka kwa BWANA.
16 Basi sasa nina haja moja ninayokuomba, usinikataze hiyo. Naye akamwambia, Sema.
17 Akasema, Nena, nakusihi, na Sulemani, mfalme, (kwa kuwa hawezi kukukataza neno), kwamba anioze Abishagi, Mshunami.
18 Naye Bath-sheba akasema, Vema; nitasema na mfalme kwa ajili yako.
19 Basi Bath-sheba akaingia kwa mfalme Sulemani, aseme naye kwa ajili ya Adonia. Naye mfalme akainuka kwenda kumlaki, akamwinamia, akaketi katika kiti chake cha enzi; kisha akaagiza awekewe kiti cha enzi mamaye mfalme; naye akaketi mkono wake wa kuume.