15 Ndipo akawaandika vijana wa maliwali wa majimbo, nao walikuwa mia mbili thelathini na wawili; kisha baada ya hao akawaandika watu wote, wana wa Israeli wote, nao walikuwa elfu saba.
16 Wakatoka wakati wa adhuhuri. Lakini Ben-hadadi alikuwa akinywa hata kulewa mabandani, yeye na wale wafalme thelathini na wawili waliomsaidia.
17 Wakatoka wale vijana wa maliwali wa majimbo wakitangulia; na Ben-hadadi akatuma watu, nao wakamwambia, Wako watu wametoka katika Samaria.
18 Akasema, Kwamba wametoka kwa amani, wakamateni wa hai; au kwamba wametoka kwa vita, wakamateni wa hai.
19 Basi wakatoka mjini hao vijana wa maliwali wa majimbo, na jeshi nyuma yao.
20 Wakapiga kila mmoja mtu wake; Washami wakakimbia, na Israeli wakawafuatia; Ben-hadadi mfalme wa Shamu akaokoka amepanda farasi, pamoja na wapandao farasi.
21 Mfalme wa Israeli akatoka, akawapiga farasi na magari, akawapiga Washami pigo kubwa.