20 Basi BWANA amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama BWANA alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli.
21 Na humo sanduku hili nimelifanyizia mahali, ambalo ndani yake mna maagano ya BWANA, aliyoyafanya na baba zetu, hapo alipowatoa katika nchi ya Misri.
22 Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake mbinguni.
23 Akasema Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote.
24 Umemtimizia mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo.
25 Na sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli machoni pangu, kama watoto wako wakiangalia njia zao, ili kuenenda mbele zangu kama wewe ulivyoenenda.
26 Sasa, Ee Mungu wa Israeli, nakusihi, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, Daudi, baba yangu.