27 Lakini Mungu je? Atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga!
28 Walakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee BWANA, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako leo.
29 Macho yako yafumbuke na kuielekea nyumba hii usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo akikabili mahali hapa.
30 Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe.
31 Ikiwa mtu amemkosa mwenzake, na kupewa sharti ya kiapo aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako, katika nyumba hii;
32 basi, usikie huko mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimpatiliza mtu mbaya, kwa kuleta njia yake juu ya kichwa chake; na kumpa mwenye haki haki yake, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake.
33 Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea tena kwako, na kulikiri jina lako wakikuomba na kukusihi katika nyumba hii;