43 basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukatende kwa kadiri ya yote atakayokuomba mgeni huyo; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe kama watu wako Israeli, nao wajue ya kuwa nyumba hii, niliyoijenga, imeitwa kwa jina lako.
44 Ikiwa watu wako watoka kwenda kupigana na adui zao, kwa njia yo yote utakayowapeleka, wakikuomba, BWANA, kuuelekea mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;
45 basi, uyasikie huko mbinguni maombi yao na dua yao, ukaitetee haki yao.
46 Ikiwa wamekutenda dhambi, (maana hakuna mtu asiyetenda dhambi), hata ukawaghadhibikia, ukawatia katika mikono ya adui zao, wawachukue mateka mpaka nchi ya adui zao, iliyo mbali au iliyo karibu;
47 basi, wakijirudia nafsi zao katika nchi ile watakayochukuliwa mateka, wakitubu, na kukusihi katika nchi ya hao waliowachukua mateka, wakisema, Tumekosa, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu;
48 watakaporejea kwako kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya adui zao, waliowachukua mateka, wakikuomba, kwa kuikabili nchi yao, uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;
49 basi, uyasikie maombi yao na dua yao, huko mbinguni, makao yako, ukaitetee haki yao;