1 Ikawa Sulemani alipokwisha kuijenga nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme, na mambo yote yaliyoingia moyoni mwake Sulemani, naye akataka kuyafanya,
2 basi, BWANA akamtokea Sulemani mara ya pili kama alivyomtokea huko Gibeoni.
3 BWANA akamwambia, Nimeyasikia maombi yako na dua zako, ulizotoa mbele zangu. Nimeitakasa nyumba hii uliyoijenga ili niweke jina langu humo milele; tena macho yangu na moyo wangu utakuwapo hapo siku zote;
4 na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu,
5 ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli.
6 Bali mkighairi, mkaacha kunifuata, ninyi na watoto wenu, msizishike sheria zangu na amri zangu, nilizoziweka mbele yenu, tena mkienda na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu,
7 basi nitawakatilia Israeli mbali na nchi hii niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa mithali na neno la tusi katika mataifa yote.