2 Kisha Daudi akamtwalia mfalme wao taji toka kichwani pake, akaona ya kwamba uzani wake ni talanta ya dhahabu, na kulikuwa na vito vya thamani ndani yake; akavikwa Daudi kichwani; akazitoa nyara za mji, nyingi sana.
3 Na hao watu waliokuwamo akawatoa, akawakata-kata kwa misumeno, na kwa sululu za chuma, na kwa mashoka. Ndivyo alivyofanya Daudi kwa miji yote ya wana wa Amoni. Nao wakarudi Yerusalemu Daudi na watu wote.
4 Ikawa baada ya hayo, kulitokea vita na Wafilisti huko Gobu; ndipo Sibekai, Mhushathi, alipomwua Safu, mmojawapo wa Warefai; nao wakashindwa.
5 Kulikuwa na vita tena na Wafilisti; na Elhanani, mwana wa Yairi akamwua Lahmi nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mti wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumaji.
6 Kulikuwa na vita tena huko Gathi; ambapo palikuwa na mtu mrefu sana, mwenye vidole vya mikono na miguu ishirini na vinne, kila mguu sita, na kila mkono sita; naye alizaliwa na Mrefai.
7 Naye huyo alipowatukana Israeli, Yonathani, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akamwua.
8 Hao walizaliwa kwake huyo Mrefai wa Gathi, nao wakaanguka kwa mkono wa Daudi, na kwa mkono wa watumishi wake.