6 Lakini Lawi na Benyamini hakuwahesabu miongoni mwao; kwa sababu neno la mfalme limemchukiza Yoabu.
7 Neno hilo likawa baya machoni pa Mungu; kwa hiyo akawapiga Israeli.
8 Naye Daudi akamwambia Mungu, Nimekosa sana, kwa kuwa nimelifanya jambo hili; lakini sasa uuondolee mbali, nakusihi, uovu wa mtumwa wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.
9 Naye BWANA akanena na Gadi, mwonaji wake Daudi, akisema,
10 Nenda ukanene na Daudi, ukisema, BWANA asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya ujichagulie moja, nikutendee hilo.
11 Basi Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, BWANA asema hivi, Kubali upendavyo;
12 miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu kuangamia mbele ya adui zako, ukipatwa na upanga wa watesi wako; au siku tatu upanga wa BWANA, yaani tauni katika nchi, na malaika wa BWANA akiharibu kati ya mipaka yote ya Israeli. Haya basi ufikiri ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.