19 Naye Shalumu, mwana wa Kore, mwana wa Ebiasafu, mwana wa Kora; pamoja na nduguze wa mbari ya babaye, Wakora; walikuwa wakiisimamia kazi hiyo ya huduma, wenye ungojezi wa malango ya maskani; na baba zao walikuwa wamesimamia matuo ya BWANA, wakiyalinda maingilio;
20 naye Finehasi, mwana wa Eleazari, alikuwa mkuu wao hapo zamani, naye BWANA alikuwa pamoja naye.
21 Zekaria, mwana wa Meshelemia, alikuwa bawabu mlangoni pa ile hema ya kukutania.
22 Hao wote waliochaguliwa kuwa wangojezi wa malango walikuwa watu mia mbili na kumi na wawili. Nao wakahesabiwa kwa nasaba katika vijiji vyao, ambao Daudi na Samweli, huyo mwonaji, walikuwa wamewaweka katika kazi yao waliyoamaniwa.
23 Basi watu hao na wana wao walikuwa na usimamizi wa malango ya nyumba ya BWANA, yaani, nyumba ya maskani, kwa zamu.
24 Hao wangojezi walikuwapo pande zote nne, kuelekea mashariki, na magharibi, na kaskazini, na kusini.
25 Na ndugu zao, katika vijiji vyao, wakaamaniwa kuingia kila siku ya saba, zamu kwa zamu, ili kuwa pamoja nao;