17 Ndipo Yese akamwambia Daudi mwanawe, Haya! Sasa uwachukulie ndugu zako efa ya bisi, na mikate hii kumi, ipeleke upesi kambini kwa ndugu zako;
18 ukampelekee akida wa elfu yao jibini hizi kumi, ukawaangalie, wa hali gani, kisha uniletee jawabu yao.
19 Basi Sauli, na watu wote wa Israeli, walikuwa katika bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti.
20 Daudi akaondoka asubuhi na mapema, akawaacha kondoo pamoja na mchungaji, akavitwaa vitu vile, akaenda, kama Yese alivyomwamuru; akafika penye magari, wakati lile jeshi walipokuwa wakitoka kwenda kupigana, wakipiga kelele za vita.
21 Nao Waisraeli na Wafilisti wakajipanga, jeshi hili likikabili jeshi hili.
22 Basi Daudi akaviacha vile vyombo vyake katika mkono wa mlinda vyombo, akalikimbilia jeshi, akafika, akawasalimu ndugu zake.
23 Hata alipokuwa akisema nao, kumbe! Yule shujaa alitokea, yule Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akitoka katika jeshi la Wafilisti, akasema maneno yale yale; naye Daudi akayasikia.