24 Basi Daudi akajificha shambani; na mwezi ulipoandama, mfalme aliketi kula chakula.
25 Mfalme aliketi kitini mwake kama sikuzote, katika kiti kilichokuwa karibu na ukuta; Yonathani alikuwa mbele yake; Abneri naye akaketi karibu na Sauli; lakini mahali pake Daudi palikuwa hapana mtu.
26 Lakini Sauli hakusema neno siku ile; maana alidhani ya kuwa, Amepatikana na neno, hakutakata; hakosi yeye hakutakata.
27 Hata siku ya pili baada ya mwandamo wa mwezi, mahali pake palikuwa hapana mtu; basi Sauli akamwambia Yonathani mwanawe, Mbona mwana wa Yese haji kula chakula, jana wala leo?
28 Naye Yonathani akamjibu Sauli, Daudi alitaka sana nimpe ruhusa aende Bethlehemu;
29 akasema, Tafadhali nipe ruhusa niende; kwa maana jamaa yetu wana dhabihu mjini mwetu; na ndugu yangu ameniamuru niende; basi sasa, kama nimeona kibali machoni pako, nakuomba, niondoke; nikawatazame ndugu zangu. Ndiyo sababu hakuja mezani pa mfalme.
30 Basi hasira yake Sauli ikawaka juu ya Yonathani, akamwambia, Wewe, mwana wa mke mkaidi, asi, je! Mimi sijui ya kuwa umemchagua huyo mwana wa Yese, kwa aibu yako mwenyewe, na kwa aibu ya uchi wa mama yako.